Na Nyeneu, P. R - Arusha
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Angellah J. Kairuki amewataka Viongozi wa Sekretarieti za Mikoa, Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na wajumbe wa timu za utekelezaji wa mradi wa BOOST kuhakikisha wanasimamia kwa ufanisi utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa elimu ya Awali na Msingi ili kufikia malengo ya serikali ya kutatua changamoto za elimu nchini.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Disemba 13, 2022 wakati akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo Makatibu Tawala wa Mikoa, Maafisa Elimu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na wajumbe wa timu za utekelezaji wa mradi wa BOOST katika Mikoa ya Singida, Manyara na Arusha, uliofanyika Jijini Arusha.
“Serikali inapimwa kwa vigezo katika kutekeleza Mradi wa BOOST nchini, sitakuwa tayari kuona fedha zimetolewa kiasi cha shilingi trilioni 1.15 na kupelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa lakini miradi haitekelezwi kwa wakati na fedha hizo kurudishwa, tutakuwa hatujatenda haki kwa wananchi” amesisitiza Waziri Kairuki
Waziri Kairuki amewataka Wajumbe wa mradi huo kuhakikisha fedha zinazotolewa katika utekelezaji wa miradi zinakamilisha miradi iliyopangwa ili kuepusha miradi mingi kutokukamilika huku fedha zikiwa zimekwisha. Vilevile amewataka wajumbe hao kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano na jamii katika utekelezaji wa mradi, pia kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika utekelezaji wa mradi ili thamani ya fedha iliyotolewa iendane na majengo yatakayojengwa ili kufikia matokeo yaliyokubalika.
Aidha, amewaagiza Wajumbe hao kuwahamasisha wazazi/walezi kuwapeleka watoto wenye umri wa kuanza shule ili waandikishwe na kuanza shule kwa wakati ili kuwaepushia mzigo walimu kwa kulazimika kurudia kufundisha mambo yale yale kutokana na wanafunzi wengine kucheleweshwa kuanza shule.
Mhe. Waziri Kairuki amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itatoa shilingi bilioni 240 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi, hivyo amewaagiza kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati kwa kuzingatia miongozo na wajiepushe na migogoro ambayo huchangia kuchelewesha utekelezaji wa miradi.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati