Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Eng. BASHIRU ROISINGISA leo Tarehe 08 Mei 2020 amekabidhi zawadi mbalimbali kwa wanafunzi walioshinda mashindano ya kubuni Alama (Monument/Icon) itakayowekwa katikati ya Mzunguko (Roundabout) katika makutano ya Barabara kuu kwenda Singida, Dodoma na Arusha.
Katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa mzunguko (Roundabout) mjini Babati makutano ya Barabara kuu kwenda singida, Dodoma na Arusha, Ofisi ya Meneja TANROADS Mkoa wa Manyara ilishirikisha uongozi wa Mkoa, Wilaya na Wadau mbalimbali na ikabuni njia ya kupata alama (Monument/Icon) muafaka itakayowakilisha mji wa Babati na Mkoa wa Manyara kwa ujumla ambayo itajengwa katikati ya mzunguko.
Njia iliyokubalika kupata alama hiyo ni kushindanisha wanafunzi kutoka shule 27 za sekondari ndani ya Wilaya ya Babati. Ambapo, mshindi wa kwanza (mwanafunzi atakayeibuka mshindi) atazawadiwa kiasi cha Shilingi Laki Tatu (300,000/=) na Shule itakayotoa Mwanafunzi itazawadiwa Shilingi Laki Mbili (200,000/=).
Katika shindano hilo lililofanyika kuanzia Tarehe 06 Februari, 2020 na kumalizika tarehe 27 Februari, 2020, mwanafunzi Rosemary Mabula wa kidato cha kwanza kutoka shule ya Sekondari Komoto ameshika nafasi ya kwanza baada ya kuibuka mshindi na kupewa Hundi (cheque) yenye thamani ya Shilingi Laki tatu na Shule kupewa hundi (cheque) yenye thamani ya shilingi Laki mbili, zoezi hilo likishuhidiwa na Afisa Elimu Sekondari (Madam Paskalina) na Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Babati.
Mwanafunzi Rosemary Mabula(Mshindi) akipokea hundi ya shilingi 300,000/=
Sambamba na hilo, Mkuu wa shule ya Sekondari ya Komoto Mr.Dennis Bakuza na Mwalimu wa Taaluma Mr.Isaya Peter walishukuru nakuahidi kuendelea kuibua vipaji mbalimbali,Afisa Elimu sekondari Halmashauri ya mji wa Babati Madam Paskalina ameishukuru TANROADS kwa kuandaa mashindano hayo na kushauri kuwa kila panapotokea fursa kama hizo wazidi kushirikiana na pia amefurahi Halmashauri yake ya Mji kuibuka kidedea kati ya Halmashauri saba za mkoa wa Manyara na kuipongeza Shule ya sekondari ya Komoto kuongoza kimkoa.