Imeandikwa na Nyeneu, P. R
Mhe. Pauline Gekul, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, leo tarehe 09 Mei 2022, amehudhuria hafla fupi ya makabidhiano ya Kompyuta kwa shule za Mji wa Babati kutoka Benki ya NMB. Makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyowakutanisha Waheshimiwa Madiwani, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Maafisa Elimu kata, Wakuu wa Shule Msingi na Sekondari yamefanyika katika shule ya Msingi Babati iliyopo Kata ya Bagara ambapo Mbunge huyo alikuwa ndiye mgeni rasmi.
Mhe. Gekul ameipongeza Benki ya NMB kwa kuwa mstari wa mbele katika juhudi za maendeleo kwa kusaidia jamii zetu kwani jamii hizi ndio zimeifanya benki ya NMB kuwa hapa ilipo na kubwa kuliko benki yoyote hapa nchini. "Kwahiyo watu wa NMB ninyi mmekuwa marafiki wema kwetu wa Jimbo hili, mmekuwa mkitupokea lakini mmekuwa mkitusaidia. Mimi ninawashukuru kama Mbunge wa Jimbo kwa niaba ya wananchi hawa", alisisitiza Mhe. Gekul
Aidha, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Bw. Dismas Prosper katika hotuba yake amesema kuwa changamoto za sekta ya elimu Tanzania kwa benki ya NMB ni jambo la kipaumbele, hii ni kutokana na ukweli kwamba elimu ndio ufunguo mkuu wa maendeleo kwa taifa lolote hapa duniani. "Tunatambua juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kusimamia upatikanaji wa elimu bora kwa nguvu zote kwa kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma hizi mjini na vijijini; hatuna budi kuipongeza Serikali kwa hilo", Aliongezea Bw. Dismas.
Benki ya NMB leo imeweza kukabidhi jumla ya Kompyuta za mezani 25 kwa shule za Msingi 09 ambazo ni Gendi, Maisaka, Darajani, Hangoni, Malangi, Himiti, Managha, Oysterbay na Babati na kwa shule za Sekondari 10 ambazo ni Nakwa, Bagara, Sigino, Kwaraa, Bonga, Himiti (Gekul), Kololi, Kwaang'w, Mutuka na Hangoni. Bw. Dismas amewaasa waliopokea vifaa hivyo kuwa kompyuta hizo zitatumika vyema kwaajili ya kuwajenga vijana na kuwapa mwanga fasaha wa kidigitali kwani ndiko ulimwengu unakoelekea. Hivyo ni vyema kuanza kuwaandaa vijana wetu na vifaa hivi vya kidigitali katika masomo yao.
Sambamba na hayo, Bw. Dismas amemalizia kwa kusema kuwa Benki ya NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wake wakubwa katika kuhakikisha kuwa changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi katika kuboresha huduma za elimu.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati