Na Nyeneu, P. R - Mjini Babati
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Lazaro Jacob Twange amewataka wajumbe wa kamati ya uelimishaji, uhamasishaji na ushirikishaji jamii (RCCE) ngazi ya Wilaya, kuhakikisha kuwa lile jukumu lao la Msingi la kuwa Daraja kati ya Watalaam Kwenda kwa Wananchi linatekelezwa kikamilifu. DC Twange ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi katika kikao maalumu cha kuwajengea uelewa wajumbe hao katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na magonjwa mengine. “Lengo mama ni lilelile la kuendelea kutii maelekezo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan la kulinda Afya za Wananchi wake ili shighuli za Maendeleo na kukuza uchumi ziendelee vizuri”. Alisisitiza DC twange.
Vilevile Mtaalamu kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Bi. Magdalena Dinawi amesema lengo kuu la kuunda kamati hii ni kuwezesha kufikisha elimu ya Afya kwa Umma kwaajili ya kuzuia magonjwa ya Mlipuko na magonjwa mengine. Baadhi ya Majukumu ya Kamati hii ni Kuwezesha, kusimamia na kusaidi kamati za Wilaya kutoa elimu ya Uchanjaji na Elimu ya Afya kwa jamii. Pia Kusambaza vipeperushi na jumbe mbalimbali kwa jamii ilioko kwenye hatari, Kusaidia na kuwezesha jamii kushiriki katika shughuli mbalimbali wakati wa majanga na dharura za afya. “Tumeona tushirikishe jamii ili kuweza kufikisha ujumbe kwa haraka”. Alieleza Mtaalamu
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Bi. Anna Fisoo amewaasa viongozi wa Dini na wataalamu wa Tiba Mbadala kuwa na mtandao wa rufaa. Pale inapotokea muumini au mgonjwa ameonekana na dalili za ugonjwa wa mlipuko mfano kipindupindu basi apelekwe au aelekezwe kufika kwenye kituo cha kutolea huduma za Afya ambacho kipo karibu ili kuzuia athari zaidi kwa wengine. Pia amewaomba wataalamu kutoka Wizara ya Afya kuendelea kutoa ushirikiano wao pale watakapohitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.
Kamati hii ya uelimishaji, uhamasishaji na ushirikishaji jamii inaundwa na Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti, Mganga Mkuu wa Halmashauri ambapo huyu ni katibu wa kamati na atakuwa na jukumu la kumpa ushauri wa kitalaam Mwenyekiti wa kamati. Mratibu wa elimu ya afya kwa umma wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Afisa Elimu wa Wilaya.
Baadhi ya Wajumbe wengine ni Afisa kilimo na Afisa Uvuvi wawili, Afisa Biashara, Mratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii, Mratibu wa elimu ya Afya Shuleni, Afisa Afya wa Halmashauri, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri, Afisa Habari wa Halmashauri. Pia, Afisa utamaduni na michezo wa Halmashauri, Wawakilishi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Mratibu wa chanjo wa Halmashauri, Kiongozi wa kijamii (mwanaume na mwanamke), Viongozi wa Dini kutoka katika madhehebu mbalimbali yaliyopo kwenye eneo husika, Waandishi wa Habari n.k.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati