Imeandikwa na Nyeneu, P. R
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Charles Makongoro Nyerere leo Novemba 30, 2021 amefanya ziara katika halmashauri mbili zilizopo katika Wilaya ya Babati. Ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Halmashauri ya Mji wa Babati. Katika ziara hiyo, RC Makongoro amekagua na kufanya ufuatiliaji katika ujenzi wa madarasa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19. Katika halmashauri ya mji wa Babati Mhe. RC ametembelea Shule ya sekondari Babati Day iliyoko kata ya Bagara ambayo inaendelea na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.
Vile vile ndani ya halmashauri ya Mji, mhe. RC ametembelea shule ya Sekondari ya Hangoni iliyopo kata ya Babati kukagua ujenzi wa Vyumba viwili vya madarasa ambapo ujenzi umefikia hatua ya kumalizia upauaji na upigaji plasta nje na ndani unaendelea pamoja na ufitishaji madirisha. Mradi wa mwisho kutembelewa ulikuwa ni ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika shule ya sekondari Nangara iliyopo kata ya Nangara. Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi nyingi sana kwani ni mradi pekee ambao umefikia hatua za mwisho kabisa za umaliziaji. Kila kitu kimeshakamilika kwa asilimia kubwa ambapo maandalizi ya upakaji rangi yanaendelea.
Katika ziara hiyo, mhe. Mkuu wa Mkoa amesomewa changamoto ambazo watekelezaji mradi wamekumbana nazo. Moja ya changamoto ni kupanda kwa gharama ya vifaa vya ujenzi. Changamoto hii imeweza kutatuliwa kwa kununua vifaa kwa ujumla na kuvitunza ndani ya stoo, ili hata gharama ya vifaa ikipanda, bado vifaa vilivyopo stoo vitaendelea kutumika. Changamoto nyingine imetajwa kuwa ni kuchelewa kufika kwa saruji ambayo ilikuwa imeagizwa kutoka kiwandani. Changamoto hii imeshughulikiwa vizuri na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mji kupitia kitengo cha manunuzi.
Picha zote na Nyeneu, P. R
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati