Na Nyeneu, P. R
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewasili Mkoani Manyara Mjini Babati leo tarehe 22 Mwezi Novemba 2022 ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya siku mbili na ya kwanza Mkoani humo na kupokelewa kwa shamra shamra kubwa na Wananchi wa Mji wa Babati.
Katika ziara yake, Mhe. Rais amezindua mradi wa Maghala na Vihenge vya kuhifadhia Chakula vinavyosimamiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) vilivyopo Mjini Babati katika Kata ya Maisaka Kijiji cha Malangi. Mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 19 hadi kukamilika. Naye Mhe. Bashe, Waziri wa Kilimo katika maelezo yake amesema kuwa malengo ya Wizara hadi kufikia mwishoni mwa Mwaka 2023 uwezo wa Nchi wa kuhifadhi nafaka ufikie tani laki tano (tani 500,000).
“Malengo yetu kufika mwezi Disemba mwaka kesho Mhe. Rais, uwezo wa nchi kuhifadhi nafaka ufike tani laki 5. Sasa hivi ulitupatia fedha tunauwezo wa kununua mazao zaidi ya tani 201,400” Akieleza zaidi Mhe. Bashe.
Aidha, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa mtandao wa Barabara za lami Mjini Babati wenye urefu wa kilomita Nane nukta moja (kilomita 8.1). Halmashauri ya Mji Babati imeweza kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya Barabara, na Kilomita 8.1 zimekamilika hadi sasa na kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 12 kwenye miundombinu pekee (Barabara, Mitaro ya maji ya mvua, Taa za barabarani 182 na njia za waenda kwa miguu), gharama za usimamizi ni shilingi Bilioni 1 na hivyo kufanya jumla ya gharama za ujenzi kuwa ni zaidi ya shilingi Bilioni 13.
Vilevile Mhe. Rais ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kuboresha miundombinu katika mji wa Babati. “Lakini mbali na uzinduzi, kuna mradi mkononi tunauchakata ambapo Babati Mji Mtapata tena Kilomita tano za lami. Tunataka Mji wa Babati uwe Mji kweli kweli, watu wafanye Biashara usiku na mchana na Mji uwe na hadhi ya Mji kweli kweli”. Amesisitiza Mhe. Rais.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Bi. Anna Fisoo kwa niaba ya Wananchi wa Mji huo, amemshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu kwa kuipatia fedha Halmashauri hiyo kwaajili ya utekelezaji wa mradi huu ambapo awali uliwekwa Jiwe la Msingi mwaka 2016 na Mhe. Rais Samia Suluhu akiwa Makamu wa Rais.
Katika taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi ameelezea namna mradi ulivyowanufaisha wananchi na kusema kuwa Mradi umewanufaisha wananchi wa Mji wa Babati na kuondoa adha ya vumbi na kupunguza adha ya mafuriko katakati ya Mji Babati na kuinua thamani ya ardhi katika Mitaa ya Oysterbay, Nyunguu, Mji Mpya, Babati Mjini na Maisaka B katika Kata za Babati na Bagara. Vilevile mradi umeongeza usalama wa waenda kwa miguu kutokana na kuwepo kwa taa za barabarani zinazoangaza wakati wa usiku na pia umewezesha kuongeza muda wa biashara ndani ya maeneo ya biashara na makazi.
Ikumbukwe kuwa, Halmashauri ya Mji wa Babati ni mojawapo ya Halmashauri 18 zilizopata fedha za Benki ya dunia na kutekeleza mradi wa kuzijengea mamlaka za serikali za Mitaa kuboresha Miji na Manispaa na Majiji nchini Tanzania ULGSP na kusimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati