Na Nyeneu, P. R
Halmashauri ya Mji wa Babati kupitia mradi namba 5441 – TCRP hadi sasa imepokea kiasi cha Tshs. 778,515,998.08 ambapo Tshs. 28,515,998 ni kwa ajili ya uhamasishaji wa chanjo na Tshs. 750,000,000 kwaajili ya miradi ya miundombinu katika sekta ya Elimu na Afya. Katika fedha hizo, Tshs. 360,000,000 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 18 sekta ya Elimu Msingi na Sekondari, Tshs. 300,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya Mji wa Babati (Emergency Medical Department) na Tshs. 90,000,000 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi 3 kwa 1 (three in one) kituo cha Afya Mutuka.
"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya; Ujenzi wa madarasa 18 umegharimu Tshs. 379,267,500 zikiwemo Tshs. 360,000,000 za Mradi na Tshs. 19,267,500 ikiwa ni Nguvu za wananachi kwa shule za sekondari za Kwaang’w (01), Mutuka (01), Sigino (01), Bonga (01), Bagara (01), Kwaraa (01), Nangara (01), F.T. Sumaye (01), Babati Day (02), Nakwa (02), Hangoni (02), Komoto (02) na vyumba viwili vya madarasa katika shule shikizi ya Sora. Ujenzi wa miundombinu hii ulianza tarehe 04.12.2021 na kukamilika kwa asilimia 100 tarehe 17.12.2021". Amesema hayo Kaimu mkurugenzi wa Mji Ndg. Faustine Masunga wakati akisoma taarifa ya makabidhiano ya mradi huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Lazaro Jacob Twange leo 28 Desemba 2021.
Katika kuwezesha utekeleaji wa mradi namba 5441 – TCRP, Halmashauri ya Mji wa Babati ilifuata hatua mbalimbali ikiwemo kuunda Kamati ya Uratibu ya Halmashauri, pia kufanya kikao cha bodi ya zaburi kuridhia mchakato wa manunuzi wa “force account” na “single source”, kufanya kikao cha kamati ya fedha na uongozi kwa niaba ya baraza la madiwani na kuridhia mpango. VIlevile kuhamasisha Baraza la madiwani kuhusu mpango na limepatiwa mafunzo rejea ya “force account”, kuunda Kamati za uratibu za Kata na kupatiwa mafunzo rejea ya “force account” na pia kuunda Kamati za miradi za “force account” katika ngazi ya Shule.
Aidha, Halmashauri ya Mji wa Babati kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa imepokea fedha toka serikali kuu jumla ya Tshs. 1,087,500,000 kwa ajili ya ujenzi ya miundombinu ya sekta ya Afya na Elimu. Ambapo Tshs. 50,000,000 ni kwaajili ya ujenzi wa jengo la Utawala shule ya Sekondari Komoto ikiwa ni awamu ya kwanza, kiasi cha Tshs. 387,500,000 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Maabara 04, Ujenzi wa Madarasa 11 katika sekta ya Elimu. Katika sekta ya Afya kiasi cha Tshs. 700,000,000 zilipokelewa kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa Zahanati ya Sigino, Chemchem na vituo vya Afya Singe, Mutuka, Singu na Maisaka.
Katika taarifa ya makabidhiano mheshimiwa mkuu wa Wilaya amesomewa faida na changamoto za mradi Namba 5441-TCRP. Faida mojawapo ya ukamilikaji wa Mradi 5441 – TCRP utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Vilevile changamoto zilikuwa ni ucheleweshwaji wa saruji mifuko 600 ambayo ilinunuliwa kwa pamoja (Bulk Purchase) kiwanda cha Dangote na pia kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi hususan vioo, Bati na Nondo.
Mheshimiwa DC amekabidhiwa rasmi jumla ya madarasa 18 ambapo kwa Shule za Sekondari ni madarasa 16 na Shule Shikizi madarasa 02 pamoja na Meza na Viti 1,600 na madawati 30 kwa ajili ya hatua zaidi.
Picha zote na Azael Amani
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati