Nyeneu, P. R - Mjini Babati
Katika kuhakikisha kuwa jamii inaelewa umuhimu wa chanjo hapa nchini, kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha wiki ya Chanjo kila ifikapo wiki ya mwisho ya mwezi Aprili ambapo kitaifa maadhimisho haya yamefanyika leo tarehe 24 Aprili, 2023 Mjini Babati Mkoani Manyara. Wiki ya Chanjo Duniani ni wiki muhimu katika kuhamasisha Wananchi wote Ulimwenguni ili wawe na uelewa na umuhimu wa Chanjo na athari zinazotokana na kukosa Chanjo ambazo ni pamoja na ulemavu wa kudumu na vifo hususani kwa watoto chini ya miaka mitano. Hayo yemesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ambaye amemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (MB) ambapo kwa mwaka huu maadhimisho yana kauli mbiu isemayo "Tuwakinge wote Kwa Chanjo” pia ikienda sambamba na ujumbe usemao “Jamii lliyopata Chanjo, Jamii Yenye Afya”.
Mganga Mkuu huyo ameendelea kusema kuwa Wizara ya Afya iliweka huduma ya Chanjo kuwa kipaumbele cha kwanza kati ya vipaumbele vyake kumi kwa mwaka 2022/2023. Katika kufikia malengo ya kipaumbele hiki, Wizara imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya huduma za afya ili kuhakikisha walengwa wote wanapata Chanjo. Dhumuni la Wizara ni kuendelea kuikinga jamii ya Watanzania dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo ambayo ni Kifua kikuu, Donda Koo, Kifaduro, Polio, Surua, Rubella, Pepo punda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo, Kichomi, Kuhara na Saratani ya shingo ya kizazi. Sambamba na Chanjo hizi, Wizara pia inatoa Chanjo za UVIKO-19 kwa watu wote wenye umri kuanzia Miaka 18 na kuendelea.
Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa Bi. Karoline Mthapula pamoja na wananchi wote wa Mkoa huo wameishukuru serikali kwa Mkoa wa Manyara kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa wiki ya Chanjo Kitaifa. “Mkoa ulipokea maelekezo kuhusu pendekezo la uzinduzi huu kufanyikia Kitaifa katika Mkoa wetu wa Manyara na tuliridhia kwa kuamini maadhimisho haya yatakuwa na faida kwetu” Alisema Katibu Tawala. Pia Bi. Karoline ameendelea kuwashukuru Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), JHPIEGO kupitia miradi ya Afya Yangu na MCGL, Clinton Health Access initiative (CHAI), Save the Children na pia kuwapongeza wananchi wote wa mkoa wa Manyara kwa namna wanavyoitikia na kutumia huduma za afya ikiwemo huduma za chanjo.
Aidha, Katika kuadhimisha Wiki hii ya Chanjo mkoa utaendelea kutoa Chanjo kwa mfumo jumuishi (integrated vaccination approach) ikijumuisha Chanjo zote katika vituo vya huduma kwa walengwa. Zoezi hili litaanza leo tarehe 24 Aprili hadi tarehe 30 Aprili katika Halmashauri zetu zote. Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara wanaitumia vizuri wiki hii kwa kuwapeleka walengwa wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupata chanjo.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati