Na Nyeneu, P. R - Babati Mjini
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Charles Makongoro Nyerere ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa huo kuendelee kudumisha ulinzi, usalama na amani ya Mkoa ikiwemo suala zima la kupinga vitendo vya ukatili ambavyo vimeshamiri katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo. Makongoro ameyasema hayo katika hafla ya kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza Miaka miwili Madarakani. Aidha, RC Makongoro amewaeleza Wananchi wa Mkoa wa Manyara mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita kwa kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa Dkt Samia.
Mhe. Makongoro amesema katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, malengo ya Serikali anayoiongoza ilikuwa ni kuhakikisha wananchi wanafikiwa na wananufaika na huduma zinazotolewa na Serikali yao. Ambapo katika kipindi chake cha miaka miwili tangu aingie madarakani Mhe.Rais ametoa jumla ya Tsh Bilioni 177.723 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo Mkoani Manyara. Miradi yote inayotekelezwa imekuwa ikielekezwa kuwanufaisha wananchi moja kwa moja kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya hadi Mkoa.
Aidha, katika Sekta ya Elimu Mkoa wa Manyara umepokea fedha jumla ya shilingi Bilioni 23.674 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo Serikali Kuu, Tozo na Uviko. Fedha hizo zimetumika kugharamia sera ya elimu msingi bila malipo, ujenzi wa vyumba vya madarasa 692, ujenzi wa matundu ya vyoo 140, maabara 21, mabweni pamoja na uanzishwaji wa shule mpya 8 za Sekondari katika Halmashauri 7 za Mkoa wa Manyara. Maboresho haya yamesaidia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu na kuongezeka kwa lengo la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza, ameeleza Mkuu wa Mkoa.
Vile vile katika sekta ya Afya Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa umepokea fedha jumla ya Shilingi Bilioni 12.430 kutoka kwenye vyanzo vya Serikali Kuu, Tozo na Uviko ambazo zimetumika katika ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba. Katika kipindi hicho vimejengwa vituo vya afya 9 vipya, zahanati 21, nyumba za watumishi 7 za 3 in 1 na ukamilishaji wa Hospitali 3 za Wilaya ya Babati, Mbulu na Simanjiro, vile vile jumla ya watumishi 327 wa afya wameajiriwa kwa lengo la kufanikisha adhma ya serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma.
Katika sekta ya Maji Mhe. Makongoro amesema Mkoa wa Manyara umepokea Bilioni 43.581 kwa ajili ya kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini unaimarika, fedha hizo zimeendelea kutumika kujenga miradi 109 ambayo kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi hiyo umesaidia kutatua shida ya Maji kwa Wananchi wa Mkoa huo iliyokuwepo hapo awali. Vilevile Mkoa wa Manyara umepokea jumla ya Shilingi Bilioni 34.013 kwaajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara za TANROAD na TARURA ambapo uboreshwaji wa barabara hizi umesaidia maeneo mengi ya vijijini kufikika kwa urahisi na kurahisisha muingiliano wa kibiashara kwa Wananchi wa Mkoa huo.
Pia, Katika Sekta ya madini Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema ujenzi wa soko la madini Wilayani Simanjiro unaendelea, hadi kukamilika utagharimu Shilingi Bilioni 5.495 na hadi sasa mradi umepokea shilingi Bilioni 1.570. Kukamilika kwa soko hili kutaimarisha biashara ya madini ya Tanzanite Mjini Mirerani, amesema Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa amesema katika kipindi hiki cha miaka miwili hifadhi za Tarangire na Manyara ambazo ni hifadhi pekee za Mkoa huo zimeweza kuingiza watalii 276,832 waliowezesha kupatikana jumla ya shilingi Bilioni 24.914. Aidha, katika kuboresha mazingira ya utalii na shughuli za kitalii, Mheshimiwa Rais ametoa kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7 kwa ajili ya marekebisho ya barabara na miundombinu ya utalii katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire; ikiwemo ujenzi wa kiwanja cha ndege hifadhini, ujenzi wa sehemu ya kupumzikia watalii na ukarabati wa barabara ndani ya hifadhi.
“Wanamanyara tunatumia fursa hii kumpongeza mheshimiwa Rais kwa ubunifu wake wa kutangaza utalii kwa kupitia filamu ya The Royal Tour.” Alieleza RC Makongoro.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati