Na Nyeneu, P. R
OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) imefanya ufuatiliaji ili kubaini namna utekelezaji wa mitaala unavyofanyika. Ufuatiliaji umeonyesha kuwa utekelezaji wa mitaala nchini kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi kidato cha sita umekuwa na tofauti kubwa katika ufundishaji na ujifunzaji wa maudhui yaliyokusudiwa kwa mwaka wa masomo husika. Baada ya tathmini; Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) wakaamua kuandaa mwongozo na kalenda ya utekelezaji mitaala katika ngazi za Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari. Mwongozo huu na kalenda ya utekelezaji wa mitaala umefanyiwa majaribio na kujiridhisha kuwa utasaidia kuwa dira ya ufundishaji na ujifunzaji nchi nzima.
Kalenda hii itasaidia katika kuleta ulinganifu wa kile kinachofundishwa kwa muda uliopangwa kwa shule zote nchini. Kalenda hii ina vipengele sita (6) ambavyo ni umahiri mkuu (mada kuu), umahiri mahususi (mada ndogo), idadi ya vipindi, mwezi, wiki na tarehe. Vipingele hivi vitamsaidia mwalimu wa somo kupanga muda wa kufundisha umahiri uliokusudiwa kwa muda muafaka. Kalenda hii itatumiwa na walimu kuandaa Azimio la Kazi pamoja na kutekeleza ujifunzaji na ufundishaji darasani kwa muda muafaka. Wasimamizi wa Elimu wakiwemo wathibiti ubora na maafisa Elimu katika ngazi ya Shule, Kata, Wilaya, Mkoa na Wizara wote watatumia kalenda hii katika kubaini umahiri wa mwalimu katika kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Halmashauri ya mji wa Babati kupitia Idara ya Elimu Msingi na Sekondari na Ofisi ya Mthibiti ubora wa Shule kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) Wilaya imeendelea kutoa mafunzo katika awamu tofauti tofauti ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni mafunzo kwa Maafisa Elimu Kata, Maafisa wengine, Walimu wakuu na Wakuu wa Shule. Awamu ya pili ni mafunzo kwa walimu wote katika Halmashauri ambapo mafunzo ya awamu ya pili yameanza tarehe 03 Februari 2022 na kuhitimishwa tarehe 04 Februari 2022.
Imeandaliwa na Nyeneu, P. R kwa msaada wa kalenda ya utekelezaji wa Mtaala wa Elimu 2022 kutoka OR-TAMISEMI na WyEST
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati