Na Nyeneu, P. R
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mheshimiwa Lazaro Jacob Twange amewaagiza Maafisa Biashara na Maafisa wote wanaohusika wakasimamie zoezi la Matumizi ya Mashine za EFD katika utoaji wa risiti. DC Twange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Kodi, ametoa maagizo hayo katika kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya ambacho kilifanyika Disemba 2, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Babati. Mhe. Twange amesema pia, Wilaya ya Babati haifanyi vizuri kwenye zoezi la utoaji wa risiti kwa mfanyabiashara na kudai risiti kwa mnunuzi. Hatua na adhabu kali zitachukuliwa kwa mfanyabiashara ambaye hata toa risiti na vilevile kwa mnunuzi ambaye hatadai risiti.
Pia Mhe. DC ameongeza kwa kuwaasa watumishi wa umma kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti pale wanaponunua kwani watumishi wa umma ndio wanufaika wa kwanza na fedha zinazotokana na kodi kupitia mishahara. "Na sisi watumishi tunajijua, hatudai risiti sisi watumishi. Kwahiyo mtazamo ukibadilika kuanzia kwa sisi watumishi wa umma tunaolipwa mishahara inayotokana na kodi, tunatakiwa tuwe mstari wa mbele kudai risiti." alisisitiza Mkuu wa Wilaya. Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema, kwa mtu yeyote atakayekamatwa kwa kosa la kutokutoa risiti au kutokudai risiti, hatokuwa mgeni wake kwa kuwa utaritibu unajulikana na unatakiwa ufuatwe bila kushurutishwa. "Naomba niseme wazi hapa, atakaye kamatwa na atakaye adhibiwa kwa kosa hili, huyu mimi sio mgeni wangu." Aliendelea kusisitiza Mhe. DC.
Mwisho, DC Twange ametoa rai kwa Wafanyabiashara kuwa watii maagizo haya ili wasiipoteze faida inayopatikana na biashara zao katika kulipia adhabu ambayo pengine imesababishwa na uzembe. "Kwahiyo wafanyabiashara kaeni vizuri, maana adhabu yenu ndo kubwa. Na mimi sioni sababu kwenye faida yako usishangae unatoa milioni tatu, milioni Nne na nusu bila utaratibu. Fedha inapatikana kwa mikakati na faida inayopatikana inatakiwa itumike kukuza mtaji wako au kuwekeza zaidi, sasa ukiwa tayari kuipoteza kwenye adhabu ambayo umeifanya kwa udhembe... sisi hatutakuwa sehemu ya kukusaidia kutatua hiyo changamoto. Pambaneni mtii sheria, toeni risiti pale mnapouza na wananchi wadai risiti wanapotoa hela zao kununua."
Picha zote na Nyeneu, P. R
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati