Na Nyeneu, P. R
Katibu Tawala Wilaya ya Babati Ndg. Halfan Matipula ameziasa Bodi na kamati ya Huduma za Afya ikiwa tu baada ya uzinduzi kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa kiwango kwa mujibu wa huduma zilizopangwa kutolewa kwenye maeneo husika. Ameyasema hayo leo tarehe 10 Mei 2021 akiwa mgeni rasmi kumuwakilisha Mkuu wa Wilaya Mhe. Jacob Twange katika uzinduzi wa bodi ya huduma za afya katika Halmashauri na kamati ya usimamizi wa Hospitali.
"Kwahiyo ninyi mnapaswa kusimamia huduma zilizopangwa kutolewa kwenye kituo cha afya, hospitali zetu zinatolewa kwa viwango ili kupunguza malalamiko ya Wananchi kwa serikali. Hilo ndo jambo la Msingi kwa sababu Serikali kuu haiwezi kusimamia kila kitu".
Aidha, Katibu Tawala amesema kuwa Mhe. Rais yeye anasema kati ya vitu ambavyo hapendi sana kuviona ni mabango ya wananchi yanayoashiria utoaji mbovu wa huduma kwa wananchi. Hivyo basi, bodi na kamati hizo zihakikishe wananchi wanapata huduma zinazotakiwa.
Katika utekelezaji wa lengo la kuboresha huduma za afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, ilitungwa sheria ya kuwashirikisha wananchi katika kusimamia huduma za Afya pamoja na kuzipa Halmashauri Mamlaka ya utekelezaji wa maboresho hayo. Maboresho yanalenga Kuhamasisha na kushirikisha Jamii katika kubuni, kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango ya Afya. Vilevile Kuziongezea Halmashauri madaraka na uwezo wa kuamua na kusimamia vyanzo vya mapato kama vile iCHF na NHIF. Hii itasaidia kupunguza pengo la mapato lililopo katika sekta ya Afya.
"Bodi na Kamati zitadumu kwa miaka 3 na Bodi inapovunjwa au kumaliza kipindi chake, itakasimu madaraka yake kwa CHMT na pia Kamati ya Usimamizi ya Hospitali ikivunjwa au kumaliza kipindi chake, timu ya Uendeshaji Huduma za Afya ya Hospitali (HMT) itakasimu madaraka ya Kamati". Alisema Mganga Mkuu wa Halmshauri ya Mji Babati Dkt. Halima Mangiri
Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria hiyo Halamashauri zimepewa mamlaka ya kuunda Bodi za Afya za Halmashauri na Kamati za Vituo vya kutolea huduma za Afya, ambapo kamati hizo zinahusishwa wajumbe wafuatao:-
Bodi hizo za afya na kamati za vituo vya kutolea huduma za afya zinakuwa na majukumu yafuatayo.
Mganga Mkuu wa Mji Dkt. Halima Mangiri (kulia) akiteta jambo na Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Jackline Goodluck wakati wa uzinduzi wa Bodi na Kamati ya usimamizi wa huduma za afya.
Bodi itawajibika kwa Halmashauri ya Mji, Jamii (kusimamia utoaji wa huduma bora za Afya) na Wajumbe wote watawajibika kwa waliowachagua. Mjumbe atakayekosa kuhudhuria vikao 3 mfululizo atakuwa amepoteza nafasi ya ujumbe. Kwa wajumbe wote wanaoingia kwa nyadhifa zao watawajibishwa kwa mwajiri kwa kuchukuliwa hatua za kiutumishi. Vile vile Bodi ya huduma za afya itakuwa na uhusiano wa kiutendaji na kamati za usimamizi za vituo. Bodi na kamati ya hospitali zitapokea na kujadili mipango ya Afya ya Halmashauri, pia itasimamia utekelezaji na taarifa ya fedha za kila robo mwaka na kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya dawa vituoni.
Katika kutekeleza majukumu yao, Bodi na kamati ya Hospitali zitakutana mara 4 kwa mwaka au zaidi pale inapobidi. Bodi haitaingilia masuala ya kiutaalam ya watumishi ili mradi wapo katika mipaka ya maadili ya kikazi. Kamati ya usimamizi ya Hospitali itawajibika kwa Halmashauri kupitia kwa Bodi ya Afya ya Halmashauri na Jamii katika kusimamia utoaji wa huduma bora za afya Hospitali.
Mwisho.
Picha zote na Nyeneu, P. R
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati