Madiwani na baadhi ya wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Babati mnamo tarehe 17 na 18 mwezi wa tano walitembelea Halmashauri za Jiji la Tanga na Mji wa Korogwe kujifunza jinsi gani Halmashauri hizo zimeweza kutekeleza miradi yake ya maendeleo.
Katika Halmashauri ya Jiji la Tanga Waheshimiwa Madiwani na Wataalam walitembelea katika stendi kuu ya Mabasi iliyopo Kange, Duka la dawa za Binadamu lililopo barabara ya nne linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji na Kituo cha runinga cha Tanga Television ambacho pia kinamilikiwa na Halmashauri ya jiji la Tanga.
Akiwakaribisha katika Jiji la Tanga Naibu Meya wa Jiji hilo Bw.Mohamed Haniu aliwaambia wadiwani na wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Babati siri kubwa ya Mafanikio katika Halmashauri yao ni kuondoa tofauti zao za kisiasa na kuwatumikia wananchi wa Tanga.”Katika Halmashauri yetu tupo madiwani wa CUF na CCM lakini ukituona tunavyofanya kazi kwa pamoja huwezi kujua diwani yupi wa CUF na yupi ni wa CCM kwani tumekubaliana kuwa Tanga kwanza vyama baadaye” alisisitiza Mheshimiwa Naibu Meya.
Akimshukuru Naibu Meya wa Jiji la Tanga Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Mh.Kibiki M.Kibiki alisema kuwa wamejifunza mengi sana katika Jiji la Tanga na watayafanyia kazi yote waliyoyapata hasahasa suala la kushirikiana bila kujali vyama walivyotoka katika kuwatumikia wananchi wa Babati.
Kuhusu stendi ya Mabasi Madiwani na wataalam wameona jinsi stendi hiyo ilivyokuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Halmashauri na kuahidi kuanza ujenzi wa stendi Mpya iliyopo eneo la Maisaka Katani haraka iwezekanavyo.
Katika Duka la Dawa za binadamu Madiwani hao waliona jinsi duka hilo linavyoweza kuwahudumia wananchi kupitia zahanati zilizopo pembezoni mwa Jiji la Tanga.
Pia walitembelea kituo cha Television cha Tanga TV kinachondeshwa na Halmshauri hiyo na kuambiwa kituo hicho pia ni chanzo cha mapato kwani kinafanya matangazo ya biashara na kurusha vipindi vya kitaalam mbalimbali kama kilimo, uvuvi, biashara n.k.
Siku ya pili ya ziara hiyo ambayo ilikuwa tarehe 18/05/2018 Waheshimiwa Madiwani walitembelea Soko kuu la Kilole na Stendi ya Mabasi ya Kilole iliyopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe na kujionea jinsi vyanzo hivyo vya mapato vinavyoweza kuchangia maendeleo ya Mji wetu kama vikisimamiwa kwa umakini.
Akihitisha juu ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati ameahidi kuisimamia Halmashauri na kushauri madiwani wenzake kushirikiana juu ya suala la kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Mji Babati ili kuacha alama kwa vizazi vijavyo.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati