Halmashauri ya Mji wa Babati imefanya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani katika Kijiji cha Nakwa Kata ya Bagara ambapo Mgeni Rasmi Katibu Tawala Wilaya ya Babati Bw. Halfan Matipula ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Babati ,Viongozi mbalimbali pamoja na Wataalam wamehudhuria maadhimisho hayo.
Maambukizi ya Virusii Vya Ukimwi {VVU} katika Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara yamepungua kutoka 2.2% mwaka 2021/22 hadi kufikia 1.8% mwaka 2022/23 na Jamii imetakiwa kuondokana na vitendo vya Unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi katika jamii zao kwa ujumla.
Katibu Tawala Wilaya Bw.Halfan Matipula amesema kuwa Serikali imeendelea kuleta mikakati zaidi ya kupambana na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu ya Ugonjwa na kutowanyanyapaa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi katika jamii. Vilevile amesisitiza wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya.Pia amewataka wazazi kutoa malezi mazuri kwa watoto wao.
Aidha Bi.Hadija Matola ambaye anaishi na Virusi vya Ukimwi amesema kuwa wanawake ni waathirika wakubwa na huu Ugonjwa hivyo amewataka kuwa mstari wa mbele katika kujikinga na maambukizi na kwa ambao hawajapima wajitokeze kupima ili kujua Afya zao.Pia amethibitisha kuwa amefanikiwa kujifungua salama mtoto wake pasipo kumuambukiza ameweza kufanya hivyo kwa kufuata maelekezo kutoka kwa Wauguzi na ameongeza kuwa jamii kwa sasa wamepata uelewa mkubwa hivyo suala la unyanyapaa limepunguza.
Pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bi. Pendo Mangali amesisitiza kuwa wazazi wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu juu ya maadili mema kwa watoto na wasiache maadili kumomomyoka katika jamii zao,wazazi wametakiwa kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa kufanya hivyo kutapunguza pia maambukizi kwa kiasi kikubwa.Ameongeza kuwa Kauli mbiu ya Mwaka huu ‘’Jamii Iongoze kutokomeza Ukimwi’’ikawe chachu katika jamii zetu juu ya suala la kutokomeza Ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi.Diana Mchonga amesema kuwa elimu inayotelewa kwa jamii imechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi kwa ujumla katika Halmashauri ya Mji wa Babati yenye Kata takribani 8 Wataalam pamoja na washauri nasaa wameendelea na zoezi la elimu juu ya upimaji na utumiaji sahihi wa dawa kwa wale wenye maambukizi na namna ya kujingika kwa ambao hawajaathirika katika jamii ikiwa ni pamoja na upimaji wa hiari wa Afya zao.
Sambamba na hilo siku hiyo imepambwa na zoezi la upandaji miti pamoja na burudani mbalimbali kutoka kwa jamii hiyo kama vile ngonjera ,mashairi, nyimbo pamoja na ngoma kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari na Msingi Nakwa pamoja na kikundi cha Ngoma cha Wagorowa Kijijini Nakwa. Na Mgeni Rasmi ametoa zawadi kwa baadhi ya washiriki waliofanya vizuri.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati