Na Nyeneu P. R
Katika kuadhimisha siku ya afya ya Kinywa na Meno Duniani, Mratibu wa afya ya kinywa na Meno mkoa wa Manyara Dkt. Pastory Mahendeka ameungana na wataalamu kutoka kitengo cha Meno Halmashauri ya Mji wa Babati pamoja na wataalamu mbalimbali wa afya kutoka Hospitali ya Mji wa Babati, leo tarehe 17 Machi 2021 wameendelea kutoa elimu mbalimbali na ushauri kuhusu afya ya kinywa na meno mashuleni, ambapo kampeni hiyo ilianza tarehe 15 mwezi Machi 2021 ikiwalenga zaidi wanafunzi wa shule za Msingi.
Daktari Mahendeka ameeleza kuwa, kila mwaka ifikapo mwezi Machi kunakuwa na wiki ya maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno ambapo maadhimisho haya yanakuwa yameambatana na utoaji wa Elimu, Ushauri, Uchunguzi na Matibabu ya Kinywa na Meno.
“Sasa katika hii wiki huwa tunafanya mambo mbalimbali ambayo yanapromote afya ya kinywa na meno. Kwa kawaida huwa tunafanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno kwa makundi mbalimbali hasa Wanafunzi, lakini pia huwa tunafanya matibabu kwa wale ambao watakutwa na matatizo, pia huwa tunatoa Elimu ya afya”. Alisema Dkt Mahendeka.
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nakwa wakiwa wamekusanyika ili kupata Elimu ya Afya ya Kinywa na meno
Maadhimisho haya yakiwa yamebeba ujumbe “Jivunie Kinywa Chako” Kitaifa yatafanyika mkoani Iringa kuanzia tarehe 15 hadi 20 Machi, 2021 ambapo wananchi wa Iringa na Mikoa jirani watapatiwa Elimu, Ushauri, Uchunguzi na Matibabu ya Kinywa na Meno katika Vituo vya Afya Ngome, Ipogolo na Hospitali ya Frelimo, Huduma ya Upasuaji na Urekebishaji Midomo wazi Itatolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Wataalam wetu wameendelea kutoa Elimu katika Shule mbalimbali za mji wa Babati ambapo leo tarehe 17 Mwezi Machi 2021 wametembelea Shule ya Msingi Nakwa iliyopo Kata ya Bagara Kijiji cha Nakwa. Kwa kutumia njia shirikishi ya ufundishaji, Wanafunzi wameelimishwa kuhusu aina za meno, kazi za Meno, Magonjwa ya Meno, namna ya kulinda meno, pia jinsi ya kusafisha meno.
Dkt Catherine Mganga kutoka kitengo cha meno Hospitali ya mji wa Babati baada ya somo la namna ya kusafisha meno na kinywa akifuatilia kwa makini zoezi alilompa mwanafunzi kueleza kwa Wanafunzi wenzake namna ya kupiga mswaki au kusafisha kinywa.
Wanafunzi hao wamejifunza pia kuwa kazi mojawapo ya meno ni kukadiria Umri, idadi ya meno yanatumika kutambua umri wa mtoto husika.
“Lakini wakati mwingine pia unakuwa hujui huyu mtoto alizaliwa lini, tunaweza kuangalia kinywani tukakadiria huyu ana miaka 16 au 17, huyu ana miaka Zaidi ya 18. Kwahiyo tunaweza kuangalia kinywani na tukakadiria umri wako”. Alieleza Daktari.
Daktari Mahendeka alisistiza Zaidi wanafunzi kulinda meno yao kwa kupunguza kula vyakula vyenye Sukari, kupiga mswaki (Kusafisha meno) angalau mara mbili kwa siku, kufanya uchunguzi wa meno kila baada ya miezi sita au mwaka mmoja. Elimu hiyo iliambatana na utoaji wa zawadi mbalimbali ikiwemo miswaki, dawa ya meno kwa wanafunzi walioweza kujibu maswali yaliyoulizwa na wataalam hao kwa ufasaha zaidi.
Sambamba na elimu hiyo ya kinywa na meno, pia wataalam wa Afya wametoa Elimu kuhusu Ugonjwa wa Korona (Covid-19) kwa wanafunzi, ambapo wanafunzi wamejifunza Zaidi maana ya Korona, namna Korona inavyoambikzwa, Dalili zake na namna ya kujikinga na Ugonjwa huo. Pia elimu ya macho kutoka kwa mtaalam wa macho Hospitali ya Mji wa Babati ilitolewa kwa wanafunzi hao kwani jicho ni moja kati kiungo muhimu sana katika Maisha ya Binadamu, pia miongoni mwa njia za kupata ugonjwa wa Korona ni Kugusa jicho (macho) na mikono iliyobeba vimelea hivyo.
Mtaalam wa Afya akiwa anauliza maswali mbalimbali yahusuyo ugonjwa wa Korona (Covid -19) kwa wanafunzi na kupewa majibu
Picha zote na Nyeneu, P. R
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati