Halmashauri ya Mji wa Babati imefanya kikao cha wadau ngazi ya Wilaya tarehe 29/07/2024 kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo [TDV 2025] na utoaji wa maoni juu ya Dira ya mwaka 2050. Kikao hicho kimeongozwa na Mhe. Lazaro J. Twange Mkuu wa Wilaya ya Babati ambacho kimehudhuriwa na Viongozi wa Chama na Serikali, Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wananchi na Wakuu wa Idara na Vitengo katika Ukumbi wa Mikutano Halmashauri ya Mji wa Babati.
Katika kikao hicho wadau wametoa maoni yao kuhusu Dira inayoisha mwaka 2025 na kuishukuru Serikali kwa kutekeleza Dira hii katika nyanja tofauti za maendeleo na wametoa maoni juu ya Dira ya mwaka 2050 kulingana na shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.
Pia Bi.Suzana Mushi mwakilishi makundi maalum ametoa maoni juu ya Ulinzi na Usalama,Virahisishi kazi na vikinga afya, Sanaa, Siasa, Miundombinu, Elimu, Uchumi, Ajira, Utamaduni na Michezo, Kundi lenye ulemavu wa afya ya akili kuwa maeneo haya yote yapewe kipaumbele katika Dira ya mwaka 2050 kwa watu wenye mahitaji maalum.
Vilevile Mwenyekiti wa kikao hicho Mhe. Twange ametoa maoni ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050 kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uwe na chanzo maalum cha mapato kitakacho wezesha Mfuko kujitegemea na kujiendesha wenyewe michango ya wanachama pekee haitoshelezi.
Aidha Mhe. Twange ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya mwaka 2050 izingatie ongezeko la watu katika utoaji wa huduma za kijamii hususani Maji kwa kila eneo kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya watu na makazi kila baada ya miaka 10.
Sambamba na hilo Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji wa Babati Bw. Florence Kundy amewashukuru Viongozi wa Serikali na Chama na Wadau wote kwa kushiriki katika kikao hicho na ameongeza kuwa wanachi waendelee kushiriki kutoa maoni kwa kutembelea Tovuti ya www.slido.com na kisha ingiza namba 1874613 au Toa maoni yako kupitia simu ya mkononi kwa kubonyeza (*152*00# >Chagua namba 8- ELIMU >Chagua Namba 4 – Dira 2050) kisha toa maoni yako.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati