Na Nyeneu, P. R
Mkuu wa Wilaya ya Babati ambaye pia ndo Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya watu na Makazi Wilayani humo Mhe. Lazaro Jacob John Twange amewapongeza Wananchi wote wa Wilaya ya Babati kwa muitikio mkubwa katika zoezi zima la Sensa, Makarani wa Sensa kwa kupita Kaya kwa Kaya, Waratibu wa Sensa na Watumishi wote ambao kwa pamoja wameweza kulifikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kufikia hatua hii nzuri tangu lilipoanza tarehe 23 Agosti 2022.
Vilevile DC Twange amesema baada ya kumaliza zoezi la Sensa ya watu siku ya jana tarehe 29 Agosti 2022, kutakuwa na Siku tatu (03) zingine kwaajili ya kuendelea na zoezi la Sensa ya Majengo kuanzia leo tarehe 30 Agosti 2022 hadi tarehe 01 Septemba 2022.
“Naomba nitoe wito kwa Wananchi wenzangu wote wa Wilaya ya Babati kama tulivyotoa ushirikiano katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililofanyika kati ya tarehe 23 hadi tarehe 29 Agosti 2022, tuendelee kutoa ushirikiano kwenye zoezi la Sensa ya Majengo linaloendelea kuanzia leo mpaka tarehe 01 Septemba 2022”. Alisisitiza Mhe. DC
Aidha Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema kuwa kama itathibitika kuwepo mtu ambaye kwa bahati mbaya hakuhesabiwa wakati wa zoezi la kuhesabu watu, anaombwa ajitokeze kutumia fursa hii kutoa taarifa kwenye Ofisi ya Kitongoji au Ofisi ya Kijiji, Ofisi ya Mtaa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri husika au atoe taarifa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya aweze kuhesabiwa ili kutimiza haki yake ya kizalendo ya kuhesabiwa.
Sambamba na yote hayo, kwa mtu ambaye atapata changamoto yoyote afanye mawasiliano yafuatayo ili aweze kupata msaada bila shida yoyote. Kama ni mkazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati piga simu kwa mratibu wa Sensa namba 0784 768 008 na kama ni mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati piga simu kwa Mratibu wa Sensa namba 0688 105 591. Kama bado utakuwa hujapata msaada tuma ujumbe kwa Mwenyekiti wa Sensa Wilaya ambayo ni 0772 906 333. Ikumbukwe kuwa zoezi la Sensa linasimamiwa kutoka katika ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Mtaa, Kata, Tarafa mpaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
“Zoezi la Sensa Wilaya ya Babati limefanikiwa vizuri na nawashukuru sana Wananchi wa Wilaya ya Babati, Makarani na Wasimamizi wote wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, mpaka hivi ninavyozungumza Wilaya ya Babati hatuna tukio lolote la kupotea kwa kifaa chochote maalumu kwaajili ya zoezi la Sensa na tunaahidi hatutoweza kupoteza kifaa chochote cha Matumizi katika zoezi la Sensa kwa sababu ni vifaa adhimu na tuna wajibu wa kuvilinda”. Alimalizia Mhe. Mkuu wa Wilaya.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati