Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji wa Babati CPA.Shaaban A. Mpendu ametoa maelezo kuhusu Uchaguzi wa Serikali za MItaa ambao unatarajia kufanyika Mwaka huu Tarehe 27/11/2024. Maelezo hayo yametolewa kwa kuwashirikisha Wadau,Viongozi,Wananchi pamoja na makundi ya watu mbalimbali katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Babati.
Msimamizi wa Uchaguzi CPA Shaaban Mpendu ameelezea matukio yote yanayotarajia kufanyika hadi hapo tarehe ya Uchaguzi utakapofanyika, Tarehe 11/10/2024-20/10/2024 zoezi la uandikishaji litaanza rasmi na vituo vitakuwa wazi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi 12:00 jioni.
Vilevile amesema kuwa Vituo vitakavyotumika kuandikishia ndio vitatumika katika zoezi la uchaguzi,na ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wakazi la kitongoji au mtaa ili waweze kushiriki kupiga kura siku ya Uchaguzi.
Aidha amesisitiza kuwa kwa wale wote wenye umri wa miaka 21 wanaotaka kugombea nafasi za Ueneyekiti wa Kijiji.Ujumbe wa Halmashauri ya Kijiji au Uenyekiti wa Kitongoji,Uenyekiti wa Mtaa au Ujumbe wa Kamati kuchukua fomu za kugombea zitakazopatikana kwenye Ofisi ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.
Sambamba na hilo amesema kuwa Vyama vya Siasa vimeruhusiwa kuweka Mawakala wakati wa uandikishaji wa wapiga kura na siku ya kupiga kura.Hivyo amewasihi wadau kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha ili wananchi wapate sifa ya kushiriki katika zoezi la uchaguzi.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati