Na Nyeneu, P. R - Mjini Babati
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bi. Anna Fisoo ameungana na watumishi kutoka Ofisi yake, Watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuendelea kuazimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo leo tarehe 20 Aprili, 2023 watumishi hao Pamoja na wafanyabiashara wa Mji wa Babati wamefanya usafi wa mazingira katika eneo la Wafanyabiashara wadogo (Machinga) ikiwa ni kuendelea kuuenzi Muungano huo. Vilevile Katibu Tawala Msaidizi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ndg. Dominick Mbwete ametoa rai kwa Wananchi wa Mji wa Babati kuwa zoezi hili la usafi wa mazingira katika maeneo yanayotuzunguka na maeneo ya baishara liwe endelevu ili kuendelea kuuweka mji wetu katika hali ya usafi wakati wote.
Shughuli hizi za usafi wa mazingira Pamoja na shughuli zingine katika maadhimisho haya zinafanyika kwa kufuatia kauli mbiu ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka huu ambayo “UMOJA NA MSHIKAMANO NDIYO NGUZO YA KUKUZA UCHUMI WETU” na vilevile kufautia maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa shughuli za maadhimisho ya sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yafanyike katika ngazi ya mikoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho hayo ambayo yameanza kufanyika kuanzia tarehe 17 Aprili, 2023 hadi siku ya kilele tarehe 26 Aprili, 2023, yatafanyika kupitia Mikoa, Taasisi za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama yataambatana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, shughuli za kijamii hususan upandaji miti, usafi wa mazingira na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali. Kadhalika, yataambatana na Mashindano ya uandishi wa Insha kwa shule za Msingi na Sekondari, mahojiano maalum na Wazee maarufu, midahalo na makongamano kuhusu Muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi sasa.
“Majengo yote ya Serikali yapambwe kwa vitambaa vyenye rangi sahihi za bendera ya Taifa, picha za Waasisi wa Muungano, Picha ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Tanzania Bara” Alisema Waziri Mkuu.
Barabara ya Babati - Singida
Sanduku la Posta: P.O.Box 383 Babati
Nukushi: +255-027-2510095
Simu: +255-027-2510095
Barua pepe: td@babatitc.go.tz
Hatimiliki@2021 Haki zote zimehifadhiwa na Halmashauri ya Mji Babati